Serif
Sans serif
Monospace

bold|normal

-2|-1|N|+1|+2

Maendeleo ya Kiswahili tangu ukoloni hadi sasa

Lugha ya Kiswahili ni kiungo muhimu sana katika maendeleo ya nchi za Afrika Mashariki hasa katika uchumi, elimu, siasa, maendeleo ya Kiswahili, utamaduni, biashara, n.k. Hivi sasa ziko juhudi za ushirikiano na maelewano kwa jamii nzima ya Afrika Mashariki kupitia lugha ya Kiswahili.

Nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki yaani Burundi, Kenya, Tanzania, Rwanda na Uganda ziko katika harakati za kuboresha muundo wa jumuia hii kwa kuangalia upya majukumu yake baada ya kuvunjika kwa Jumuia ya Afrika Mashariki takriban miaka 20 iliyopita. Idadi ya wanachama imeongezeka kutoka nchi tatu za Kenya, Tanzania na Uganda na kuwa nchi tano baada ya nchi za Rwanda na Burundi kujiunga na Jumuia hii.

Mojawapo ya mambo muhimu yaliyokubaliwa na viongozi wa nchi hizi yalihusu suala zima la lugha ambalo litasaidia kurahisisha mawasiliano baina ya wananchi wa nchi hizi kuanzia ngazi za chini kwa wananchi wa kawaida hadi ngazi ya juu kwa viongozi wakuu. Lugha ya Kiswahili ilipewa nafasi kubwa ya kuweza kutumika kama lugha ya mawasiliano miongoni mwa nchi zote za Jumuia hii.

Itakumbukwa kuwa wakati wa enzi ya ukoloni wa Uingereza ilikuwapo kamati ya lugha ya nchi za Afrika Mashariki iliyojulikana kama Kamati ya Lugha (Kiswahili) ya Afrika Mashariki. Lugha ya Kiswahili ilipewa nafasi kubwa tangu mwaka 1930 wakati kamati ilipoanzishwa hadi mwaka 1964 kamati ilipovunjika. Kamati ilipovunjika mwaka 1964 baada ya kila nchi kupata uhuru wake, Tanzania ndiyo iliyokuwa mwenyekiti wa mwisho wa kamati na hivyo kuendelea kutekeleza baadhi ya majukumu ya Kamati hadi leo chini ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ambayo iko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) imefanyiwa mabadiliko ya muundo wake kiutendaji na sasa inafahamika kama Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI). Taasisi ya TATAKI sasa imekuwa ni muunganiko wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili na Idara ya Kiswahili zote cha Chuo Kikuu cha UDSM. Idara ya Kiswahili iliyokuwa inajishughulisha na ufundishaji wa Kiswahili kwa wanachuo wa digrii ya kwanza, ya uzamili na uzamivu.

Kamati ya Lugha (Kiswahili) ya Afrika Mashariki ilikuwa na utaratibu wa kukutana kwa zamu katika nchi wanachama kama ifuatavyo:

Tangu mwaka 1964 baadhi ya shughuli za kamati ziliendelea kusimamiwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI). Kutokana na kila nchi kupata uhuru wake, mfumo wa sera ya lugha uliachwa nchi wanachama jukumu la kuendeleza lugha ya Kiswahili. Mwaka 1967 Tanzania ilianzisha Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) kwa lengo la kukuza, kuendeleza na kuratibu maendeleo ya Kiswahili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Majukumu ya Bakita yalitekelezwa vilivyo hasa suala la kusanifu lugha ya Kiswahili na kutayarisha istilahi za masomo mbalimbali kama Kemia, Fizikia, Hisabati, Utawala, Siasa, Elimu, n.k. Hatua ya pili ni kutayarisha kamusi za istilahi hizi kazi ambayo imekamilishwa na TUKI.

Mwaka 1970 TUKI iliwekwa chini ya mamlaka ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati kilipoanzishwa rasmi. Hadi sasa taasisi hii iko chini ya chuo hicho.

Mwaka 1999 viongozi wa Jumuia ya Afrika Mashariki walikutana na kuona umuhimu wa kuwa na chombo kimoja rasmi ambacho kazi zake ni kukuza, kuendeleza na kuratibu Kiswahili katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla. Chombo hiki kinajulikana kama Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki chenye malengo ya kuwezesha kukuza siasa, uchumi, maendeleo ya jamii, elimu, utamaduni, sayansi na teknolojia katika eneo la Afrika Mashariki.

Dira ya Kamisheni hii ni kuwa chombo mahususi cha kukuza, kuratibu na kuendeleza Kiswahili kwa ajili ya maendeleo ya uchumi, siasa, utamaduni, elimu kwa nchi wanachama.

Makao Makuu wa Kamisheni hii yatakuwa Zanzibar na mipango ya kuwapata viongozi wa Kamisheni inaendelea.

Shabaha za Kamisheni:

 1. Kuimarisha mawasiliano kitaifa, kikanda na kimataifa katika kukitumia Kiswahili.
 2. Kukikuza Kiswahili kama lugha ya kanda kwa kuzingatia tunu kama usawa, uwiano, haki za binadamu na demokrasia.
 3. Kuanzisha, kusaidia na kuhimiza maendeleo ya Kiswahili katika Jumuia ya Afrika Mashariki.
 4. Kuhimiza ushirikiano katika utafiti na vituo vya elimu ya juu kwa mafunzo ya Kiswahili na utafiti.
 5. Kuzisaidia nchi wanachama kutoa elimu ya juu ya Kiswahili kwa walimu na mawasiliano kwa jamii kwa jumla.
 6. Kufanya marekebisho ya mitalaa na kuongeza ujuzi katika masomo ya fasihi na isimu kulingana na mahitaji ya jamii ya Afrika Mashariki.
 7. Kuendeleza ubora wa Kiswahili katika kuhuisha lugha ya Kiswahili na programu za elimu. Mitalaa ihakikishe kuwa ufundishaji na utafiti katika Kiswahili unafikia kiwango kinachokubalika.
 8. Kuzisaidia nchi wanachama kwa maendeleo ya watu binafsi na uendeshaji wa asasi za Kiswahili.
 9. Kuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya kimataifa kuhusu Kiswahili na kuziarifu nchi wanachama. Kuhimiza ubadilishanaji wa wafanyakazi na wanafunzi miongoni mwa asasi za Kiswahili.
 10. Kuchunguza, kufuatilia, kuhuisha na kuhimiza maendeleo ya Kiswahili kwa ajili ya upashanaji habari, mawasiliano, shughuli za kiteknolojia na matumizi ya lugha.
 11. Kuwezesha na kuratibu tafsiri kwa Kiswahili kwa nchi wanachama na vyombo vingine vya kimataifa.

Usanifishaji wa Kiswahili

Mojawapo ya shughuli za Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki ni kusanifu maneno mapya pamoja na kuoanisha maneno ya zamani ili yatumike kwa ajili ya kuimarisha maelewano baina ya nchi zote za Jumuia ya Afrika Mashariki. Kikwazo kilichokuwapo hapo awali ni kutoikuza lugha ya Kiswahili kwa kiwango cha kimataifa kwa upande wa taaluma ya sayansi na kiteknolojia. Bingwa na mtaalamu aliyebobea katika Kiswahili Profesa Ali Mazrui aliwahi kusema kuwa sera ya elimu na ya lugha ya Kiswahili havikupewa kipaumbele katika ukuzaji wa sayansi na teknolojia. Ukosefu wa istilahi za Kiswahili katika sayansi na teknolojia umesababisha walimu na wahadhiri kupata matatizo katika kuandika vitini na vitabu vya sayansi kwa lugha ya Kiswahili.

Kihistoria nchi za Kenya na Uganda zimetegemea sana istilahi zilizotayarishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), Taasisi ya Ukuzaji Mitalaa (TIE), Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (IAE) na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita).

Hata hivyo, katika ngazi ya vyuo vikuu, wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vikuu vya Kenya, wamekuwa na mawasiliano ya karibu ya kitaaluma baina yao kwa kubadilishana taaluma mbalimbali. Mfano mzuri ni wakati UNESCO/SIDA walipofadhili semina kuhusu masuala ya usanifishaji wa istilahi za Kiswahili mwaka 1989. Wanataaluma wengi kutoka Kenya walihudhuria semina hii na huu ukawa ni mwanzo nzuri wa ushirikiano katika kukuza lugha ya Kiswahili kwa kiwango cha vyuo vikuu.

Utayarishaji wa Istilahi

Inasemekana kuwa watumiaji wa istilahi za Kiswahili ni kwa ajili ya wanataaluma na si kwa watu wa kawaida. Kwa hiyo wataalamu wanaotaka kuandika vitabu au vitini vya kufundishia masomo ya sayansi wanazo istilahi za kuwawezesha kukamilisha azma zao. Wataweza kutumia istilahi zilizotayarishwa na Bakita na kuchapishwa katika kitabu cha Istilahi za Kiswahili cha mwaka 2005 na machapisho mengine yanayoweza kupatikana Bakita na Tuki. Iko mifano michache ya wanataaluma wa masomo ya Kemia na Hisabati waliowahi kuandika miswada ya masomo hayo kwa Kiswahili katika kiwango cha elimu ya kidato cha tano na sita wakitumia istilahi ambazo zimetayarishwa na Bakita. Kwa bahati mbaya wachapishaji wa vitabu walishindwa kuchapisha miswada ya vitabu hivyo kutokana na kutokuwapo kwa sera kamili ya lugha ya Kiswahili katika shule za sekondari.

Bakita walitayarisha istilahi za aina mbalimbali kwa kutumia njia zifuatazo:

 1. Upatikanaji wa maneno kutoka katika lugha za kigeni hasa Kiingereza ambayo ni kwa mtindo wa kutohoa. Hii ina maana kuwa maneno ya kigeni yanaandikwa kwa mfumo wa tahajia ya Kiswahili kwa kuzingatia matamshi ya Kiswahili. Kwa mfano katika utohozi tunapata maneno kama:
  Kiingereza Kiswahili
  atom
  adapter
  battery
  speaker
  transformer
  atomi
  adapta
  betri
  spika
  transfoma n. k.
  Istilahi hizi huandikwa kwa kutumia misingi ya Kiswahili inayozingatia misingi ya mofolojia ya Kiswahili. Mojawapo wa misingi hiyo ni kwa kumalizia neno kwa kutumia irabu isipokuwa maneno machache yasiyoishia na irabu kama mathalan, takriban na hususan.
 2. Njia nyingine inayotumika ili kuwa istilahi za Kiswahili ni kwa kupata maneno kutokana na visawe mbalimbali vya Kiswahili. Kwa mfano:
  ship
  capital
  plans
  equality
  meli
  mtaji
  mpango
  usawa n. k.
 3. Njia ya tatu ni kwa kukopa maneno kutoka katika lugha za asili badala ya kutoka katika lugha za kigeni kama Kiingereza, Kiarabu, Kireno , Kihindi, n.k.
  Kwa mfano yako maneno ya kikabila yaliyochangia kupata istilahi za Kiswahili kama:
  Ikulu (Kinyamwezi) = State House
  Kitivo (Kipare) = Faculty
  Mbuti (Kimasai) = Duodenum
  Kisabeho (Kipemba) = Breakfast dish
  Uloto (Kizaramo), = Bone marrow
  Msigano (Kiyao/Kihaya) = Inequality
  Upepo nyiri (Kipare/Kihaya) = Jet-stream
  Ubigiaji = (Kibondei) = Reafforestation, n.k.
 4. Kuunganisha maneno mawili na kuunda neno moja jipya, (Compouding of words). Kwa mfano:
  prehistory
  labour force
  appendix
  triangle
  back sight
  fungicide
  boar
  saw
  historiakale
  nguvukazi
  kidoletumbo
  pembetatu
  kipimonyuma
  kiuakuvu
  nguruwedume
  nguruwejike n. k.

Hii ni mifano michache ambayo imetumika katika kuongeza istilahi za Kiswahili katika juhudi za kupata maneno mapya ya sayansi. Inawezekana ziko njia nyingine ambazo wataalamu wetu wa Kiswahili watabuni ambayo yatasaidia kukifanya Kiswahili kiweze kumudu maendeleo ya sayansi na teknolojia. Jambo la msingi ni kwa serikali kutoa fedha za kutosha kwa watafiti wa lugha ya Kiswahili kuweza kufanya utafiti wa kina katika lahaja za Kiswahili kama Kiamu, Kingazija, Kitumbatu, Kihadimu, Kimvita, n.k. pamoja na lugha zetu za asili ambazo ni hazina kubwa katika ukuzaji wa Kiswahili.

Kwa mujibu wa Sera ya Elimu ambayo imetoka hivi karibuni, upo mpango wa muda mfupi, wa kati na muda mrefu wa kukiwezesha Kiswahili kuwa ni lugha ya kufundishia katika mfumo mzima wa elimu kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu. Lengo ni kuhakikisha kuwa masuala ya sayansi na teknolojia yanapata nafasi yake katika maendeleo yetu kwa kutumia Kiswahili. Maandalizi yanayotakiwa kufanywa ni kama kuandika vitabu na vifaa vingine vya kujifunzia na kufundishia na pale inaposhindikana kutafsiri kutoka lugha za kigeni. Pia kuwaandaa walimu hata wale wa kigeni watakaokuja kufundisha hapa nchini . Suala la msingi ni kwa viongozi wetu kubadilika kifikra na kuona kuwa kukitumia Kiswahili si kujidhalilisha bali ni kupiga hatua kimaendeleo katika sayansi na teknolojia kwa taifa letu. Matumizi ya lugha za asili katika elimu ni dhana inayokubalika kwa nchi nyingi duniani kama vile Kenya. Je, ni nini mwelekeo wa Tanzania?

stephenjmmaina1965@yahoo.com

Источник: http://www.mwananchi.co.tz/